Makundi ya vijana yanahusika katika zoezi la kusafisha mazingira katika eneo la Changamwe wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kubuni sheria maalum itakayowawezesha kulipwa pindi wanapotekeleza usafi huo wa mazingira.
Wakizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Vijana hao waliitaka serikali ya kaunti kuwaboreshea mazingira ya utenda kazi kwa kuwapa vifaa hitajika, sare za kazi, pamoja na msaada wa aina yoyote utakaowawezesha kujikimu kimaisha.
Akiyapokea mapendekezo ya jumla ya makundi 18 ya vijana chini ya mwavuli wa ‘Mwema’, mwakilishi mteule wa Kaunti ya Mombasa Mary Akinyi alisema kwamba mapendekezo ya vijana hao yatawasilishwa kwa idara husika ya mazingira katika kaunti hiyo, kwa lengo la kuwawezesha vijana hao kutekelezewa matakwa yao.
Akinyi alisema kwamba serikali ya kaunti hiyo ina jukumu la kutumia uwezo wake katika kuimarisha maisha ya vijana kwa kuyahusisha katika kazi mbalimbali za mikono sambamba na kuwakimu na zabuni tofauti ili wanufaike na kuwepo kwa serikali za kaunti.
"Ningependa kuwaambia kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho iko na uwezo wa kuwapa vijana ajira na swala hilo nitaliwasilisha kwa idara husika na mtasaidiwa,” alisema Akinyi.
Mwakilishi huyo maalum katika Bunge la Kaunti ya Mombasa amekiri kwamba swala la uchafuzi wa mazingira ni changamoto ya jadi katika Kaunti hiyo ya Mombasa, hali inayopaswa kutatuliwa.