Vijana na wanawake katika Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kujitenga na tabia ya kusubiri kuajiriwa na badala yake kujihusisha na maswala mbalimbali yatakayowawezesha kubuni ajira.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa wa Nyanjani katika Shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre, Mwalimu Rama, amesema kuwa ili vijana na wanaweke kukabiliana na changamoto za maisha, sharti wawe wabunifu wa ajira.

Akizungumza katika kongamano la vijana na wanawake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rama alisema kuwa iwapo vijana na wanawake watakubali kujishughulisha na ubunifu wa ajira, basi swala la umaskini na ukosefu wa ajira litapungua kwa kiwango kikubwa.

Rama alisema kuwa kama shirika watahakikisha kuwa wanawahamasisha vijana na wanawake Mombasa kuhusu kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa kujihusisha na ajira ndogondogo kama vile biashara za mboga na ufugaji.

“Kama shirika tumeamua kuwahamasisha vijana na wanawake kufahamu maswala ya kujiajiri na kuepukana na changamoto za ukosefu wa ajira. Lazima tutazishinikiza idara mbalimbali katika Kaunti ya Mombasa kutoa zabuni ili vijana na wanawake kujiajiri,” alisema Rama.