Vijana katika eneo la Pwani wamehimiza kujiunga katika makundi ili kufaidika na mipoko inayotolewa na serikali.
Katibu mkuu katika Wizara ya huduma kwa umma, vijana na jinsia nchini Zeinab Hussein, amesema kuwa kuna umuhimu wa vijana kusaidiwa kupata fedha hizo ili kuwawezesha kujiendeleza kimaisha.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Changamwe mjini Mombasa, katika halfa ya kuwakabidhi vijana na akina mama fedha za kujiendeleza kimaendeleo, Zeinab alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni 17 zingali katika hazina ya wizara hiyo.
Alisema kuwa fedha hizo zinahitajika kutolewa kwa vijana kufanya miradi.
Katibu huyo alisema kuwa vijana wengi hawajafahamu umuhimu wa kuekeza katika benki za kijamii.
Aliahidi kutuma maafisa wa wizara hiyo kuwahamasisha vijana ili kuhakikisha kuwa wanajiendeleza kimaisha na kukuza uchumi wa nchi.
"Asilimia kubwa ya vijana katika eneo la Pwani hawajajiunga na makundi ya maendeleo ili kupata fedha kutoka kwa serikali. Tuko hapa kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kutumia fedha hizo kujiendeleza kimaisha,” alisema Zeinab.
Wizara hiyo imekabidhi hazina ya fedha ya akina mama shilingi milioni 209, ile ya vijana shilingi milioni 99 na hazina ya Uwezo ikipewa shilingi milioni 246.