Mwakilishi wa wadi ya Sensi iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Nyagaka Saisi Onchong’a amewaomba vijana kutoka wadi yake kuungana pamoja na kuunda vikundi ili kukabidhiwa mikopo kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo kama njia moja ya kujiendeleza kimaisha na kuinua uchumi wa kaunti hiyo.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano afisini mwake iliyoko mjini Kisii, mwakilishi huyo aliomba vijana wote kutoka wadi ya Sensi kujiunga kwa vikundi ili kukabidhiwa mikopo ya kufanyia biashara pamoja na kuinua uchumi wa kaunti ya Kisii.
“Sisi wawakilishi wa wadi tulipitisha mswada wa kutenga pesa za mikopo ambazo vijana na akina mama watatukuwa wakikabidhiwa ili kufanyia biashara. Serikali yetu iliposoma bajeti ya kaunti, pesa za mikopo zilitengwa ili wananchi kuchukua na kufanyia bishara,” alisema Ochong’a.
Aliongeza: “Vijana wakizembea bila kufanya kazi hawatakula. Ndio maana tunaomba kila kijana awajibike kikamilifu kwa kufanya biashara.”
Aidha, mwakilishi huyo amesema vijana wanaweza kujiendeleza kwa kufanya biashara badala ya kutegemea pesa kutoka kwa wanasiasa huku akisema umaskini utapunguzwa katika kaunti ya Kisii ikiwa kila mwananchi atawajibika vilivyo kwa kufanya biashara.
“Naomba kila mtu katika wadi yangu atumie pesa za kaunti kwa kutengeneza pesa zingine,” alisema Nyagaka.