Vijana kutoka maeneo Bunge yote katika Kaunti ya Kisii wameombwa kujiunga na vikundi mbalimbali vitakavyowawezesha kupata viangua mayai incubators ili kuanza mradi wa ufugaji kuku na kujiendeleza kimaisha na kuinua viwango vya kilimo.
Akiongea siku ya Jumatatu katika hafla ya kutoa pesa za mikopo kwa baadhi ya vikundi kutoka Kaunti hiyo, Katibu katika Wazara ya Ugatuzi na Mipangilio ya Serikali Ann Waiguru aliwaomba vijana hao kujiunga katika vikundi ambavyo vitawazesha kuendelea kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Kulingana na Katibu Waiguru, Serikali Kuu imetoa viangua mayai viwili kwa kila eneo Bunge katika Kaunti ya Kisii vitakavyopewa kwa vikundi vya Vijana.
“Serikali imetoa viangua mayai viwili kwa kila eneo Bunge, sasa ni wajibu wa Vijana kujiunga katika vikundi ili wapokezwe viangua hivyo ili kujiendeleza kiuchumi,” alisema Katibu Waiguru.
Baadhi ya vijana walioudhuria hafla hiyo waliukumbatia mradi huo na kusema wako tayari kujiunga katika vikundi mbali mbali ili kupokezwa viangua hivyo.
“Niko tayari kujiunga katika kikundi ili kunufaika na mradi huu wa Serikali kwa kuwa ufugaji wa kuku hasa katika maeneo yetu huwa ina faida kubwa,” alisema Mogeni Nyamamba mmoja wa vijana waliopokewa mkopo huo.
Aidha, Nyamamba amewaomba vijana wenzake kuchukulia mradi huo kuwa wa umuhimu kwa vijana na kujiunga na vikundi ili kunufaika na mradi huo.
Kulingana na Nyamamba vijana wakijiunga katika vikundi watapata jambo la kushughulikia na kuwa na kazi ya kufanya bila kurandaranda mitaani.