Vijana katika ukanda wa Pwani wametahadharishwa dhidi ya kutumiwa na viongozi wa kisiasa ili kuzua vurugu katika makongamano ya kisiasa yanayozidi kuchacha eneo la Pwani.

Share news tips with us here at Hivisasa

 Afisa wa maswala ya vijana katika shirika la kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ eneo la Pwani Mwalimu Rama, alisema kuwa vijana wamekuwa wakitumiwa na wanasiasa ili kuvuruga mikutano ya wapinzani wao hali ambayo inahatarisha usalama.

Akizungumza katika kongamano la vijana la amani katika eneo la Bombolulu mjini Mombasa siku ya Alhamis, Rama alihoji kwamba kwa muda mrefu sasa vijana wamekuwa wakihadaiwa na viongozi wa kisiasa na ni lazima hali hiyo ibadilike.

Rama alisema kwamba shirika hilo litazidisha makongamano yake kuhusu vijana na uongozi pamoja na kudumisha amani katika Ukanda wa Pwani ili kuona kwamba kuna mabadiliko makubwa katika maswala ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

"Tumekuwa vijana wengi wamekuwa wakitumiwa na viongozi wa kisiasa ili kuzua vurugu wakati wa mikutano ya kisiasa na kusababisha uhasama baina ya viongozi na jamii kwa hivyo sisi tunataka vijana wabadilike na wao pia watafute nyadhfa za uongozi nchini ili kubadilisha fikra zao potovu," alisema Rama.

Mwanaharakati huyo wa vijana katika ukanda wa Pwani aliwataka vijana kujiandaa vilivyo na kuingia uongozini bila ya kuwajali wababe wa kisiasa wa eneo la Pwani.