Vijana katika eneo bunge la Bahati wametakiwa kutoharibu maisha yao ya mbeleni kwa kujiingiza katika utumizi wa madawa ya kulevya.
Mwakilishi wa Wadi ya Bahati katika bunge la kaunti ya Nakuru, Peter Nderitu, alimewataka vijana kujihusisha na mambo yatakayoongeza dhamani katika maisha yao.
Akiongea siku ya jumanne alipokagua miradi iliyoanzishwa na vijana kupitia hazina ya uwezo katika wadi yake, Nderitu alisema kuwa vijana wanafaa kutumia ujana wao katika kuweka msingi dhabiti wa maisha kwani huo ndio wakati mwafaka.
Aliwakumbusha kuwa watakuwa watu wasiokuwa na umuhimu katika jamii iwapo watajiiingiza katika utumizi wa dawa za kulevya.
“Hakuna kitu kizuri utakachopata kwa kutumia mihadarati ila ni kuharibu maisha yako mwenyewe. Badala ya kuharibu mda na pesa katika ulevi, ni vyema utumie pesa hizo na muda huo katika kufanya mambo yatakayoboresha maisha yako,” alihoji Nderitu.
“Wakati wa kuweka msingi wa maisha yako ni sasa na mkumbuke kuwa ujana utakuja na kuenda,” alisema Nderitu.
Aliwataka vijana kukumbatia masomo ili waweze kupambana vyema na wenzao katika ulimwengu wa sasa.
“Huwezi kushindana na wengine katika dunia ya sasa bila masomo, na kwa hivyo, hata mnapoendelea na miradi yenu pia mkumbuke umuhimu wa masomo kwa sababu hata kusimamia miradi kama hii kunahitaji kisomo,” alisema mwakilishi huyo.