Vijana kutoka ya kaunti za Kisii na Nyamira wamehimizwa kujiandikisha katika taaluma mbali mbali zinazohusiana na ukarabati wa barabara na ujenzi wa miundomisingi ili kunufaika na kazi za ujenzi wa miundomsingi unaoendelea.
Msimasimazi mkuu wa taasisi ya mafunzo ya uhandisi na ukarabati wa barabara (Kenya Institute of Highway and Building Technology, KIHBT) mjini Kisii David Manyara amewahimiza wakazi kujifaidisha na kuwepo kwa taasisi hio katika eneo hilo.
Bwana Manyara alishangazwa na idadi ndogo ya wanafunzi kutoka kaunti hizo, ambao wamekuwa wakijiandikisha ilhali taasisi hiyo iko katika kaunti ya Kisii.
Alisema kwa miaka mingi taasisi hiyo imekuwa ya manufaa kwa vijana kutoka kaunti zingine kote nchini. Alisema kuwa wengi wa vijana ambao wamekuwa wakijiunga na taasisi hiyo wamekuwa wakipata ajira katika kampuni kubwa za ujenzi.
Aliwakumbusha hasa jamii mbalimbali kutoka kaunti hizo mbili za Gusii kutumia nafasi ambayo imejitokeza kupitia katika shirika moja lisilo la kiserikali la kutoka nchi ya Japani ambalo linafahamika kama Community Roads Empowerment (CORE).
"Shirika hili liliweza kuwafadhili zaidi ya vijana 400 katika matumizi ya teknolijia ya kisasa ya kukarabati barabara ya DO-NOU," alisema.
Aliwashauri kuwa sasa itakuwa rahisi kwao kufaidi kwa kupata kazi kupitia katika shirika la CORE ambalo linatarajiwa kuanzisha miradi ya kujenga barabara kwa kutumia teknolojia hiyo kwenye kaunti zote nchini Kenya.
Alisema kuwa vijana wengi wakijipatia mafunzo hayo watapata fursa ya kuajiriwa na kampuni hiyo kwa muda mrefu.