Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Vijana katika eneo la Komarock, Matungulu wamejipatia njia nyingine ya kupata pesa kwa kusukuma magari yanayokwama kwenye maji.

Vijana hawa waliokusanyika katika kundi la vijana watano hungoja magari yanayopita katika barabara ya kutoka Komarock kuelekea Kenol ili kupatiana usaidizi wao kisha kulipwa.

Wakiongozwa na mmoja wao Felix Kaseve, walieleza mvua iliyonyesha siku mbili mfululizo iliharibu barabara inayosababisha magari mengi kukwama katika eneo hilo huku ikibidi wenyewe kuomba usaidizi.

Kaseve alieleza kuwa kila gari ndogo linalipa shilingi mia moja huku magari makubwa yakilipa shilingi mia mbili ili vijana hawa kuweza kusaidia kusukuma.

"Barabara hii ni mbaya haipitiki lakini magari mengi hayana budi ila kuipitia,” alisema Kaseve.

“Baada ya kupatiana usaidizi wa bure kwa kusukuma magari yaliyokwama tuliona tunaacha fursa ya kupata hela kupita na hivyo tukaamua kulipisha," aliongezea.

Aidha, madereva wanaotumia barabara hio waliiomba serikali ya kaunti hio kushughulikia swala hili haraka ipasavyo kwani imekuwa shida kuu.

Hii ni baada ya malori ya kubeba changarawe na makaa kukwama na kutatiza biashara huku wasafiri wakilazimika kulipa mara mbili ya nauli ya hapo awali.