Mara nyingi watu wanapopata elimu na kuajiriwa maeneo mbalimbali husahau mitaa waliyozaliwa na kuanza maisha mapya sehemu tofauti.
Mambo ni tofauti katika mtaa wa Magongo mjini Mombasa ambapo kundi moja la wakaazi waliozaliwa katika mtaa huo waliamua kuja pamoja na kuanza miradi ya kusaidia jamii.
Mwanzilishi wa kundi hilo la Magongo Re-Union, Lilian Japani, amesema walitumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp kuungana pamoja.
“Tulianza na Facebook alafu tukaingia kwa WhatsApp. Hapo tulikuwa tunaunganisha wale watu wote ambao walizaliwa na kusomea hapa Magongo,” alisema Japani.
Kundi hilo lenye zaidi ya washirika 30 liliamua kuanzisha mpango wa kusafisha mazingira eneo hilo huku wakihusisha vijana na wanawake.
Vile vile, vijana hao hutembea nyumba hadi nyumba wakizungumza na wakaazi na kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira safi.
Patrick Wanguche, mmoja wa vijana hao alisema waliamua kuanzisha mpango huo baada ya kuona kwamba watu wengi hasa vijana wanajihusisha tu na starehe na kusahau usafi wa mazingira, huku shughuli hiyo wakiachia wanawake.
“Inasikitisha kuona kwamba tunazingatia zaidi kutafuta pesa, kutafuta chakula na kupeleka watoto shule lakini hili swala la kutunza mazingira tumeacha kabisa,” alisema Wanguche.
Kundi la Magongo Re-Union lilianzishwa tarehe 18 mwezi Julai mwaka huu, na sasa wanalenga kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo, sio tu mtaa wa Magongo peke yake bali Mombasa na Pwani kwa ujumla.
Aidha, vijana hao walisema kuwa kazi yao ni ya kujitolea na wanafurahi kwamba vijana wengi sasa wameanza kujitokeza ili kuunga mkono mpango huo.