Vijana wengi katika kaunti ya Uasin Gishu wameonyesha hamu yao ya kujiunga na huduma ya polisi kupitia zoezi la uchaguzi wa polisi litakalofanyika tarehe 20 mwezi huu kote nchini .
Naibu OCPD katika kituo cha polisi cha Eldoret magharibi Tom Achiya, amethibitisha kuwa kuna idadi kubwa ya vijana wanaofika katika ofisi yake kuomba fomu za kujiunga na huduma hiyo.
“Vijana wengi wametembelea ofisi yangu kuuliza fomu za maombi, lakini nimekuwa nikiwaelekeza kutembelea tovuti ya huduma za polisi ili kuzijaza fomu hizo. Hii ina maana kuwa kuna vijana zaidi ambao wana nia ya kujiunga na huduma hii,” alisema Achiya.
Achiya pia aliongeza kuwa ongezeko la idadi ya vijana tayari kujiunga na jeshi wamethibitisha wakfu wao wa kulinda nchi.
Pia alisema kuwa licha ya wakati mgumu unaokabili nchi, inatia moyo kujua kwamba bado kuna wale wananchi ambao wana nia ya kujitolea kulinda taifa.
“Kuongezeka kwa idadi ya wanotaka kujiunga na kikosi cha polisi ina maana kwamba vijana wako tayari kuiwakilisha Kenya. Hii ni uwakilishi mzuri wa utaifa,” alisema naibu OCPD.
Achiya aliongezea kuwa ajira itafanyika kwa namna huru na haki, huku akionya wale ambao wana mpango wa kushiriki katika ulaghai kuwa watapigwa marufuku, kukamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.
"Uchaguzi utafanyika kwa haki, uovu wowote au ufisadi utashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria,” alisema Achiya.