Vikao vya bunge la Kaunti ya Mombasa kwa mara nyingine vilikosa kufanyika licha ya taarifa za awali kuripoti kuwa vikao hivyo vingerejelewa siku ya Jumanne.
Inaripotiwa kuwa wawakilishi wadi hao bado hawajarejelea uwiano baina yao, jambo lililomsababisha spika wa bunge hilo kukosa kuviitisha vikao kwa hofu ya kutokea mfarakano mengine.
Hata hivyo, Karani wa bunge hilo, Salim Juma, kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, alikanusha madai hayo, na kusema kuwa hadi sasa hajaibainaiki ni lini vikao hivyo vitarejelewa.
“Sina uhakika vikao vitarejelewa lini lakini nina imani kuwa haitachukua muda kwani wawakilishi wadi wameonyesha nia ya kuweka kando tofauti zao ili kuwahudumia wananchi,” alisema Juma.
Aidha, Juma alikanusha madai kuwa vurugu zilizoshuhudiwa katika bunge hilo zilitokana na tofauti baina ya wawakilishi wadi wanaomuunga mkono Gavana Hassan Joho na Seneta Hassan Omar.
“Wabunge wote ni wa mrengo wa Cord hivyo haiwezikani kuwa kuna mirengo miwili tofauti baina yao. Hizo zilikuwa tu tofauti za binadamu za kawaida,” alisema Salim.
Katika majuma mawili yaliyopita, bunge la Kaunti ya Mombasa lilikumbwa na vurugu baada ya wawakilishi wadi kurushiana makonde katika jaribio la kutaka kumuondoa mamlakani Spika wa bunge hilo Thadius Rajwayi.