Kamati ya kuchunguza wizara ya fedha na utajiri wa maafisa wake katika kaunti ya Kisii imeanza kazi yake jinsi ilivyoratibiwa hapo mbeleni.
Hii ni baada ya wanakandarasi wa kaunti ya Kisii kutuma ombi kwa kamati hiyo kuchunguza jinsi wizara hiyo imekuwa ikipeana kandarasi na kuchunguza utajiri wa maafisa hao jambo ambalo sasa limeitikiwa.
Akizungumza siku ya Jumanne mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchunguzi Charles Nyagoto alisema uchunguzi huo umenza ili kubaini na kuhakikisha uwazi kwa wakaazi wa Kisii.
“Vikao vya uchunguzi wetu vilianza Jumanne na mwenyekiti wa wanakandarasi katika kaunti ya Kisii Kennedy Mariera alikuwa wa kwanza kufika mbele yetu ili kupeana ushahidi alionao kuhusu wizara hiyo na maafisa wake, uchunguzi ungali unaendelea,” alisema Nyagoto.
Wakati huo huo, Nyagoto aliomba wale wana ushahidi wowote kuhusu wizara hiyo kufika mbele yake ili ukweli wa mamxbo uweze kubainika.