Vikao vya kujadili maendeleo vimeanza rasmi katika Kaunti ya Mombasa, huku wakaazi wa Changamwe wakionekana kuchangia kwa kutoa maoni yao kuhusu miradi mbalimbali ambayo serikali ya kaunti imeanzisha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada ya Gavana Hassan Joho kuwataka wakazi kujitokeza kwa wingi kwenye vikao hivyo.

Wakazi wa Changamwe walijitokeza kwa wingi siku ya Alhamisi kushiriki majadiliano hayo, huku maswali mengi yakiibuka kuhusiana na bajeti ya mwaka 2016/2017, iliyoleta hali ya mgawanyiko miongoni mwa viongozi.

Mathew Fondo, mkazi wa Bangla huko Changamwe, alisema maswala yote yanayohusiana na bajeti ni muhimu na sharti yashughulikiwe kwa muda unaofaa.

Kwa upande wake, Mwanaisha Hamisi, alilaumu serikali ya kaunti kwa kuchelewesha miradi muhimu kama vile ya kuunganisha mabomba ya maji.

Hamisi alisema kuwa wakazi wengi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa maji safi ya kunywa na kulingana na bajeti ya mwaka, mradi wa kusambaza maji eneo hilo ulipaswa kukamilika mwakani, ila kufikia sasa wanakandarasi waliopewa jukumu hilo bado hawajaanza kutekeleza kazi hiyo.

Wakaazi hao wametaka kufafanuliwa miradi yote ambayo kaunti hiyo imeanzisha na pia kushirikishwa wanapohitajika kufanya maafikiano.

Kwa upande wake, afisa mkuu wa mawasiliano wa kaunti Richard Chacha amewahakikishia wakazi kuwa maswala yote ya kifedha yatashughulikiwa vilivyo kulingana na sheria.

“Hakuna lolote litakaloamuliwa pasi kutohusishwa kwa wakazi wa Mombasa,” alisema Chacha.