Walimu wakuu katika shule za msingi zilizoteuliwa kwa kufanyia majaribio mpango wa vipakatalishi katika kaunti ya Mombasa wanatoa wito kwa serikali kuharakisha mpango huo ili kuregesha imani kwa wanafunzi na wazazi.
Walimu hao wanasema tangu shule hizo kuchaguliwa katika majaribio ya mpango huo bado vifaa hivyo havijaletwa licha ya serikali kuahidi kufanya uzinduzi huo hivi karibuni.
Wiki kadhaa zilizopita Waziri wa Habari na Mawasiliano Joe Mucheru alitangaza kwamba serikali itaanza shughuli ya kutembelea shule 150 zilizochaguliwa katika majaribio hayo ili kuzikagua iwapo zimejitayarisha vya kutosha.
Katika kaunti ya Mombasa shule 4 zilibahatika kuchaguliwa katika mpango huo ikiwa ni pamoja na shule ya msingi ya Mwijabu, Port Reitz, Spaki na Kisauni.
Akiongea siku ya Jumanne shuleni mwake, mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mwijabu Kibibi Masoud alisema kuwa serikali ilianza kutangaza kuleta vifaa hivyo lakini inashangaza kwamba bado ahadi haijatimizwa.
“Tunashukuru shule yetu ilichaguliwa lakini sasa tangu wakati huo bado wanafunzi wanangoja bila kuona lolote na wazazi pia hawaelewi kinachoendelea,” alisema Kibibi.
Mapema wiki hii maafisa kutoka wizara ya elimu walitembelea shule kadhaa mjini Mombasa na kutathmini hali ya shule hizo katika zoezi lililoanza wiki jana likitarajiwa kukamilika katika kipindi cha wiki mbili baada ya shule zote kutembelewa kote nchini.
Sasa walimu hao wanasema ikiwa zoezi hilo litacheleweshwa basi huenda Wakenya wakakosa imani na mpango huo wa serikali ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitoa ahadi wakati alipochaguliwa.
Kulingana na wizara ya elimu ni kwamba baada ya zoezi la kukagua shule hizo kikamilika vifaa hivyo takribani 1100 vitaanza kutolewa kuanzia mwezi Juni katika awamu ya kwanza kabla awamu ya pili mwaka ujao.
Hata hivyo mwalimu Kibibi aliongeza kuwa sharti serikali ihakikishe kwamba kuna usalama wa kutosha katika shule hizo pindi itakapotoa vifaa hivyo na kusaidia katika kuvirekebisha vinapoharibika kwani itakuwa gharama kubwa kwa shule.