Shirika moja lisilo la kiserikali kwa jina Vision Fund limewapa mikopo vikundi saba ili kuanza biashara na kujiendeleza kimaisha.
Kila kikundi kilipata shilingi milioni moja kama njia moja ya kupunguza hali ya umaskini katika eneo la Kisii.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Ogembo, eneo bunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, mwenyekiti wa shirika hilo Lumumba Nyaberi alisema umaskini utapunguzwa katika eneo la Kisii ikiwa watu watafanya biashara za aina yote ili kupata riziki ya kila siku.
Mwenyekiti huyo aliomba wakazi kuungana pamoja na kuunda vikundi ili nao waweze kujinufaisha kwa kupata pesa za mikopo na kufanyia biashara.
Alisema sharti wawe na umoja kama wanahitaji kujiendeleza kwa kikundi na wawe na maendeleano kati yao wenyewe.
“Sioni haja ya mtu kuendelea kuwa maskini maana siku hizi mikopo ambayo itawasaidia kujiendeleza ipo. Hakuna haja ya kusalia kuteseka katika jamii kutokana na umaskini,” alisema Nyaberi.
Wakazi walioshuhudia vikundi hivyo vikikabidhiwa mikopo walisema kuwa kujihusisha na vikundi ni jambo la busara huku wengi wakiapa kuunda vikundi ili waweze kukabidhiwa mikopo na kufanya biashara.
“Tuliposhuhudia vikundi vikikabidhiwa mikopo ndipo tulipogundua kuwa mtu akiwa katika kikundi ni njia mojawapo ya kupata pesa za kufanya biashara. Mimi mwenyewe nitajiunga kwa kukundi ili niwe nikifanya biashara,” alisema Jackline Osanse mkazi.
Aidha, Lumumba Nyaberi aliwaomba watu kutoogopa kuchukua mkopo kwa kuhofia kurudisha pesa kwa shirika hilo huku akiwaambia kuwa wanaweza kufanya biashara na kurudisha zile walizokabidhiwa na kubaki na faida.