Viongozi wa kidini katika kaunti ya Garissa wameilaani na kutoa msimamo mkali dhidi ya wanawake waislamu wanaotumia bodaboda kama njia ya usafiri.
Wakiongea katika hafla ya kuchangisha pesa kwa madarasa moja katika eneo la Sambul, imamu wa msikiti ya Al Rahma, Sheikh Hussein, alisema kuwa hatua ya wanawake wa kiislamu kutumia bodaboda kama usafiri ni haramu katika sheria ya kiislamu na kwamba wataendelea kukipiga vita vitendo hivyo.
“Dini na sheria ya uislamu imeharamisha wanawake waislamu kupanda bodaboda wanaposafiri ndani ya mji wa Garissa na sisi kama viongozi wa kidini tutalipiga vita usafiri huo,” alisema Hussein.
Viongozi hao waliitaka serikali ya kaunti ya Garissa kuchukua hatua mwafaka ya kudhibiti mwendo wa kasi unaoendeshwa bodaboda hizo ikizingatiwa kuwa ajali nyingi zinasababishwa na bodaboda kwa kuwa usafiri wao ni rahisi na wa bei nafuu.
“Tunataka serikali ya kaunti ya Garissa kuhakikisha kuwa wanapunguza ajali zitokanazo na usafiri wa bodaboda. Hatutaki kuona raia wa Garissa wakiangamia,” aliongezea Hussein.
Tangu biashara za bodaboda ziingie mjini Garissa, imeshuhudiwa usafiri wa kutoka eneo moja hadi lingine likirahisishwa na idadi ya wanawake wa kiislamu wanaotumia kuongezeka maradufu haswa nyakati za usiku, hivyo kufanya viongozi wengi mjini kukana na kupiga vita usafiri wa bodaboda.