Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amewaonya wazazi walio na desturi ya kukimbilia viongozi wa siasa wanawao wanapotiwa nguvuni kwa kukiuka sheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Nassir amesema kuwa wengi wa wazazi katika maeneo yanayotajwa kukumbwa na utovu wa usalama wana mazoea ya kutembelea viongozi na kuwarai kuwasaidia kwa mchango wa dhamana, ambayo mara nyingi huhitajika katika mahakama ili wanao waachiliwe huru.

Akizungumza kwenye mkutano uliowaleta pamoja viongozi mbalimbali ikiwemo Kamishna wa Mombasa Maalim Mohamed katika makao makuu ya polisi mjini Mombasa, Nassir alisema kuwa wakati umefika kwa viongozi wote kuungana na idara za usalama ili kuimarisha hali ya usalama.

Mbunge huyo alisema kuwa imekuwa tatizo kwa baadhi ya wafanyabiashara kuendesha shughuli zao nyakati za usiku.

Akitoa mfano wa mama mmoja aliyemrai kumsaidia ili amwokoe mwanawe aliyekuwa amekamatwa na maafisa wa usalama kwa tuhuma za kushiriki wizi wa mabavu katika eneo la Mvita, Nassir alisema kuwa wazazi wanapaswa kuchunguza mienendo ya wanawao na pia kuwafundisha maadili mema ili waweze kuepukana na vitendo viovu katika jamii.

Aidha, ameitaka idara ya usalama kusimama kidete na kurudisha hadhi ya Kaunti ya Mombasa kama kivutio cha watalii.