Viongozi kutoka Kaunti ya Kisii wametofautiana kuhusu uteuzi wa raisi Uhuru Kenyatta wa wasimamizi na wanachama katika bodi mbali mbali nchini.
Akiongea na waandishi, aliyekuwa diwani na ambaye ni mshirikishi wa chama cha Ford-People katika kaunti ya Kisii, Steve Arika, alichangamkia kuchaguliwa kwa wakisii katika bodi hizo, huku akiwasuta wanaoingiza siasa katika uteuzi huo.
Arika alihoji raisi alizingatia makabila yote nchini kwani aliwazawadi hata wapinzani wake, inayodhihirisha kuwa hana ukabila.
“Sisi kama jamii ya wakisii tunaunga mkono uteuzi wa raisi. Inaonyesha anatupa shukrani kwa kummunga mkono katika uchaguzi uliopita. Aidha, hiyo haimaanishi kuwa ni ukabila ama kuwatunuku waliomuunga mkono, kwani hata wapinzani wake haswa wale wa mrengo wa CORD wamenufaika,” alisema Arika.
Kwa upande mwingine, mwakilishi wa wadi ya Bokimonge inayopatikana katika eneo bunge la Bomachoge Borabu, George Bibao, ameonyesha kutoridhika na uteuzi huo kwa kuwa kulikuwa na mapendeleo kwani hakuna aliyeteuliwa kutoka kaunti yao ndogo.
“Tunafurahia uteuzi wa raisi na kuwakumbuka wakisii, lakini hakuzingatia usawa wa kimaeneo kwani hakuna aliyeteuliwa kutoka eneo bunge letu. Hiyo haimaanishi ni ukabila ama ukoo, bali tungefurahia kuwakilishwa na mmoja wetu katika uteuzi huo,” alihoji Bibao.
Miongoni mwa walionufaika kutoka Kisii ni waliokuwa wabunge Dkt Robert Monda na Walter Nyambati miongoni mwa wengine.
Uteuzi alioufanya raisi Uhuru Kenyatta mnamo siku ya Jumatatu ambapo aliwateua wasimamizi na wanachama 302 katika bodi mbalimbali nchini, unaendelea kuzua mseto wa hisia huku wapinzani wakisema uteuzi ulichochewa kisiasa.
Aidha, wanaoegemea upande wa serikali, wanampongeza raisi kwa uteuzi huo.