Viongozi wa Kaunti za Kisii na Narok wanatarajiwa kufanya mkutano wa amani kesho Jumanne, katika mpaka wa Kaunti hizo mbili, kujaribu kutafuta suluhu la mgogoro wa wizi wa ng’ombe uliyofanyika wiki jana.
Hii ni kulingana na Kamishina wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi, ambaye amesema watafanyia mkutano huo katika Wilaya ya Kenyenya sehemu ya Kiango, inayoshuhudia mapigano ya jamii mbili zinazoishi katika mpaka huo.
“Tunatarajia kufanya mkutano wa amani katika mpaka wa kaunti ya Kisii na ya Narok ambapo viongozi kutoka pande mbili husika tutakutana kutafuta suluhu kwa mgogoro baina ya jamii za wakisii na wamaasai baada ya ng’ombe kuibwa na kupotelea eneo la Trans Mara,” Mwangi alithibitisha.
Aidha, Mwangi amethibitisha kuwa hadi sasa, ni mtu mmoja ameaga dunia huku watano wakiuguza majeraha, na wengine wakikadiria hasara baada ya mimea na nyumba zao kuharibiwa.
Mkutano huo utawajumuisha viongozi wa siasa kama Gavana wa Kisii James Ongwae, na Mwenzake wa Narok Samwel Ole Tunai, na wengine pamoja na viongozi wa utawala wa mkoa kutoka pande zote mbili.
Mzozo ulizuka tarehe tatu wiki jana wakati wezi wanaoshukiwa kutoka upande wa jamii ya wamaasai walivuka mpaka na kuiba ng’ombe mmoja kutoka Kijiji cha Nyabitumiwa, kilichoko Kaunti ya Kisii, iliyowapelekea wenyeji kufwata ng’ombe wao lakini nyayo zikapotelea katika kijiji cha Shankoi.
Mapigano yalizuka na licha ya viongozi wa pande zote mbili kujaribu kuyasitisha, haikufaulu, iliyopelekea serikali za kaunti mbili kutuma vikosi vya usalama kushika doria.
Inasemekana mtu mmoja aliuliwa na polisi alipokuwa anatoroka licha ya utawala wa mkoa kumtetea mwenzao kuwa, marehemu alikuwa anawakabili polisi.