Kamanda wa polisi wa kawaida katika kaunti ya Kisumu Nelson Njiiri, ametoa wito kwa viongozi wa kidini watakaoandaa kesha za kuamkia mwaka mpya wa 2015 kuhakikisha kuwa wanashirikiana na maafisa wa polisi kuimarisha usalama wa waumini wao.
Kwenye mahojiano na mwanahabari wetu afisini mwake siku ya Jumatano, Njiiri alisema kuwa viongozi wa makanisa vile vile wanapaswa kuhakikisha kuna walinzi wa kutosha, kwa kukodesha huduma za walinzi wa kampuni za kibinafsi.
Njiiri amewataka madereva wawe waangalifu, akionya wamiliki wa magari dhidi ya kuendesha magari kiholela na kwa mwendo wa kasi.
Ametoa tahadhari kwa yeyote atakayepatikana akienda kinyume cha sheria kwa kisingizio cha ulevi, na kusema kuwa ataadhibiwa kwa mjibu wa sheria.
“Tulikuwa na Krisimasi njema juma lililopita na ni wakati wa kuukaribisha mwaka mpya pia kwa njia salama. Idara ya polisi imeweka mikakati mwafaka ya usalama wa kila mtu, ila kila mmoja ana jukumu la kufanikisha usalama wake,” alisema Njiiri.
Amesema kuwa kila mwananchi ana haki ya kusherehekea kufika mwaka mpya wa 2015, lakini lazima sherehe hizo ziandaliwe pasi na kukiuka haki za watu wengine.
Viongozi wa makanisa mbali mbali jijini Kisumu, watandaa kesha Jumatano usiku kuukaribisha mwaka mpya.
Wakenya wa matabaka mbali mbali, wanatarajiwa kukesha makanisani na majumbani, wakisali, kuimba, kusifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia afya na uwezo wa kufika mwaka 2015.