Viongozi wa kisiasa hususan katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kutoingiza siasa katika suala la Shamba la Waitiki, na badala yake kuwashauri wakaazi hao kulipa ada ya shilingi milioni 182 kama livyopendekeza serikali.
Mshirikishi mkuu wa utawala katika ukunda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa azmio la serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mkenya anapata hati miliki ya ardhi ili kusitishwa masuala ya uskwota hususan katika eneo la Pwani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Marwa alisema kuwa serikali ilitenga shilingi elfu moja kila mwezi kwa kila familia iliyopewa hati miliki hiyo, ada ambayo italipwa kwa kipindi cha miaka 10 hadi 12.
Aliema kuwa hati miliki hizo ni halali na wakaazi wanaweza kuzitumia kupata mikopo kutoka kwa benki.
"Tunawaomba viongozi wa kisiasa kutoingiza siasa katika suala la Shamba la waitiki. Pesa ambayo serikali imetenga wakaazi walipe kila mwezi ni kidogo sana. Jamani sio kila kitu tunaweka siasa. Tuwache pia Wakenya wafaidike na mambo mengine,” alisema Marwa.
Afisa huyo aliwata wakaazi waliyofaidika na hati miliki hizo zilizotolewa na Rais Uhuru Kenyatta alipozuru eneo la Pwani katika ziara yake ya kutekeleza ajenda za serikali kupuuzilia mbali matamshi ya viongozi hao na kujali maisha yao ya baadaye.