Viongozi katika eneo la Pwani wametuma risala zao za rambi rambi kwa familia ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa kumpoteza mkewe Bi Lucy Kibaki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Wakiongozwa wa Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir siku ya Jumanne, viongozi hao wamesema kuwa wamepokea taarifa hiyo ya kufariki kwa Mama Lucy kwa mshtuko mkubwa na kuwataka Wakenya kuzidi kuiombea familia ya Kibaki.
Viongozi hao wamesema kuwa Wakenya wanafaa kuungana na familia hiyo katika maombi hasa wakati huu mgumu wakuomboleza huku wakizidi kuwahimiza wananchi kuungana na kudumisha amani nchini.
Viongozi hao ni pamoja na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko.
"Tumepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa lakini tunazidi kuiombea familia ya mheshimiwa Mwai Kibaki tukimtakia nguvu hasa wakati huu mgumu,” alisema Nassir.