Viongozi mjini Naivasha sasa wanawataka wawekezaji na wanakandarasi wanaofanya kazi katika eneo hilo kuzihusisha jamii katika miradi yao.
Aidha, viongozi hao waliutaja mradi wa kujenga reli ya kisasa -SGR- kama moja wa zile ambazo zinafaa kutwaa nafasi tele za kazi kwa vijana wa eneo hilo.
Haya yaliibuka wakati wa mkutano uliowaleta pamoja zaidi ya wakaazi 500 katika ukumbi wa mikutano wa kanisa la ACK Jumatano mjini humo kuhusu nafasi za kazi zilizoko katika eneo hilo.
Kiongozi mmoja, Wachira Wairegi, alisema kuwa: “Ni jambo la kusikitisha kuona nafasi za kazi katika eneo hili zikipewa watu wengine kutoka kaunti za nje na kuwaacha wakaazi wa hapa wakitaabika.”
Naye Mwangi Muraya alisema,“Ni bayana kuwa asilimia 70 ya nafasi za kazi zinafaa kuwaendea wakaazi wa eneo hili na wala si wale wa kutoka nje.”
Kiongozi wa chama cha Jubilee kaunti ya Nakuru James Karimi na madiwani wa kaunti hiyo Simon Wanango na Esther Njeri ni kati ya wale ambao walihudhuria mkutano huo.