Viongozi wa kidini, kisiasa na kitamaduni mjini Naivasha wameungana na wenzao katika ngazi ya kitaifa kushtumu matamshi ya Seneta wa Machakos Johnson Muthama wakimtaka kuomba radhi wanawake nchini.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa JAP tawi la Nakuru James Karimi, viongozi hao wamesema kuwa kiongozi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko anafaa kumchukulia hatua Muthama bila ya kuchelewa.
Akiongea wakati wa mkutano wa chama hicho katika hoteli ya Jazz mjini Naivasha siku ya Jumatatu, Karimi alidai kuwa seneta huyo amekuwa akitoa matamshi ya kuleta uchochezi kwenye mikutano ya hadhara na hakuna chochote kimefanywa dhidi yake.
Akizungumza katika eneo tofauti, aliyekuwa mbunge wa Naivasha na waziri msaidizi wa mazingira Jane Kihara, alisema Muthama anapaswa kuwaomba wakenya na haswa akina mama msamaha.
"Seneta Muthama anapswa kuheshimu jamii na kuomba akina mama msamaha kufuatia matamshi yake,” alisema Bii Kihara.
Naye Pharis Ndung'u kutoka baraza la wazee wa Naivasha alisema kwamba wananchi katika kaunti ya Nakuru wataandamana hadi kwake nyumbani ili awaeleze ni kwanini alitoa matashmi kama hayo dhidi ya rais.
"Muthama ajue wakzi wa kaunti ya Nakuru wataandamana hadi kwake nyumbani, atueleze kwanini hamweshimu rais, na kama hataki tufanye hivyo, aombe msamaha,” alisema Ndung'u.