Wakazi wa wadi ya Rigoma, Kaunti ya Nyamira, wamewarai viongonzi wote kuheshimiana na kuungana ili kuleta maendeleo katika kaunti hiyo.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatatu katika wadi ya Rigoma, wakazi hao wakiongozwa na Brian Ogero walisema kuwa umoja na heshima miongoni mwa viongozi ndio utaleta maendeleo katika Kaunti ya Nyamira.
Wakazi hao waliwaomba viongozi wote kuanzia gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kushirikiana na wabunge, wawakilishi wa wadi, mwakilishi wa wanawake na seneta ili kuleta maendeleo.
“Naomba viongozi wote waungane na waheshimiane ili waweze kuleta maenedeleo yale waliyotuahidi wakati wa kampeini,” alisema Brian Ogero, mkazi wa Rigoma.
Ombi la mkazi huyo Brian liliungwa mkono na idadi kubwa ya wakazi ambao walikuwa katika eneo hilo waliowaomba viongozi walio katika mamlaka kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe ili kaunti hiyo iweze kusonga mbele kimaendeleo.
Wakati huo huo, wakazi hao waliomba viongozi wa Kaunti ya Nyamira kuheshimu viongonzi wenzao walichochaguliwa ili kutekeleza maendeleo pamoja kikamilifu.
“Tunaomba viongozi wote kuungana na kuheshimiana ili watufanyie maendeleo,” alisema, Jane Osante mkazi.
“Sisi sote tunaomba maendeleo kama wanataka heshima kutoka kwetu. Ikiwa hawataleta maendeleo tutaendelea kuwakosoa kila wakati,” alisema James onsarigo mkazi.