Maafisa kutoka kwenye Wizara ya Ugatuzi na Mipangilio ya Serikali wamepiga kambi katika mkahawa mmoja mjini Nyamira kufanya kikao na mawaziri pamoja na makatibu wao, kuwafunza kuhusiana na matumizi mazuri ya fedha kwenye wizara zao.
Akihutubu kikao cha wanahabari siku ya Jumatano baada yakuwakaribisha rasmi maafisa hao, Katibu wa Kaunti ya Nyamira Erick Onchana alisema kwamba kongamano hilo litahakikisha kuwa utendakazi wa viongozi mbalimbali unaimarika hata zaidi.
"Kongamano linaloendelea kwenye mkahawa huu ni lakuhakikisha kwamba mawaziri, makatibu wao na wakurugenzi mbalimbali wanapata hamasa yakuimarisha utendakazi wao hata zaidi," alisema Onchana.
Onchana aliongeza kwa kusema kuwa kongamano hilo linafuatia makubaliano ambayo mawaziri na makatibu wa kaunti waliyoyaafikia pamoja na wawakilishi wadi kwenye hafla ya mashauriano kule Itibo.
Akizungumzia swala la kuhamasisha maafisa wakuu wa serikali ya Kaunti ya Nyamira, Onchana alisema kuwa serikali ya Kaunti hiyo ikiongozwa na Gavana John Nyagarama imeweka mikakati kabambe kuhakikisha kuwa maafisa hao wanapewa motisha kutekeleza majukumu yao.
"Serikali ya kaunti hii imeweka mikakati kuhakikisha kuwa maafisa wetu wanapata hamasa kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” aliongezea Onchana.