Huku ikiwa imesalia siku moja pekee kabla ya kukamilika kwa zoezi la kusajili wapiga kura, viongozi kadhaa wanaendelea kushinikiza Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kuongeza muda zaidi.
Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Lamu Shakila Abdalla ameitaka tume hiyo kuongeza muda zaidi, na kusema kuwa zoezi hilo linafaa kuendelea kila siku kulingana na sheria ya uchaguzi.Shakila amesema ni haki ya kila Mkenya kujiandikisha kama mpiga kura wakati wowote.“Ongezeni muda ili watu wajiandikishe kwa wingi, ni haki yao,” alisema Shakila.Kauli sawa na hiyo ilitolewa na wafuasi wa chama cha Jubilee eneo la Pwani, waliosema kuwa bado wanaendeleza kampeni za kuwarai wananchi kujitokeza na kusajiliwa.Wakiongozwa na Peter Ponda, viongozi hao walisema kuwa muda uliobaki unaweza leta mageuzi katika uongozi wa kaunti endapo wananchi watajitokeza kusajiliwa.“Iwapo Wakenya watajitozeka kwa wingi kwa kipindi kilichobaki, basi tutaweza kuleta mageuzi makubwa,” alisema Ponda.Haya yanajiri baada ya mwenyekiti wa Tume ya IEBC Wafula Chebukati kusema kuwa tume hiyo haitaongeza muda zaidi, na kuwataka Wakenya kujisajili kabla ya zoezi hilo kufika tamati.
Maelezo ya picha: Maafisa wa Tume ya IEBC wakiwasajili wapiga kura hapo awali.
Picha/standardmedia.co.ke