Ziara ya Naibu Rais William Ruto katika eneol la Pwani mwishoni mwa juma imeonekana kuupa nguvu mrengo wa Jubilee kisiasa huku baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo waliochaguliwa kwa tiketi ya muungano wa Cord wakiapa kujiunga na upande wa serikali. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na mbunge wa Lunga Lunga Khatibu Mwashetani, Gideon Mung'aro wa Kilifi kaskazini na Mustapha Iddi wa Kilifi kusini, viongozi hao wanasema wakati umefika kwa eneo la Pwani kuwa ndani ya serikali.

''Hatutakubali kuwa nje ya serikali tena, tutaungana pamoja tujenge chama kimoja cha Jubilee tuwe ndani ya serikali 2017,'' alisema Mwashetani. 

Kauli yake iliungwa mkono na aliyekuwa mbunge wa Changamwe Ramadhan Kajembe aliyesema chama cha ODM kimepitwa na wakati na hakina lolote jipya la kuwapa wakazi wa Pwani. 

Kwa upande wake Ruto, akizungumza mjini Malindi siku ya Jumapili, aliwahimiza viongozi hao kujiunga na upande wa ushindi ili wabuni serikali 2017. 

''Safari hii tunataka serikali inayojumuisha viongozi wote kutoka tabaka zote nchini, kwa hivyo shikilieni msimamo wenu,'' alisema Ruto. 

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga na Peter Shehe wa Ganze. wote wanaougemea mrengo wa Cord. 

Eneo la Pwani kwa mara nyingi limekuwa ngome ya upinzani, lakini safari hii huenda mambo yakabadilika kufuatia idadi kubwa ya viongozi wake kutangaza kuunga mkono mrengo wa Jubilee katika uchaguzi wa 2017.