Viongozi tofauti kutoka chama cha Cord wameikosoa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kwa kutupilia mbali sahihi zilizokusanywa na chama hicho kwa madhumuni ya kuifanyia mabadiliko katiba kupitia mswada wa Okoa Kenya.
Akizungumzia katika hafla ya mazishi ya binamuye eneo la Uamanai seneta wa kaunti ya Machakos Johnstone Muthama alisema kuwa tume ya uchaguzi isipopitisha sahihi ilizowasilishwa nazo chama cha Cord kitalazimika kuichukulia hatua za kisheria.
Aidha Muthama alimsuta kiongozi wa wengi katika bunge Aden Duale pamoja na mwenyekiti wa chama cha TNA kwa kutoa tuhuma kuwa sahihi zilizowasilishwa na chama hiki zilikusanywa kwa njia za magendo.
Muthama alidai kuwa tume hii imeonyeshana wazi kuwa sio huru kama inavyodai kwani inaonekana ikiegemea upande was chama cha Jubilee.
Muthama aliapa kumuunga mkono kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka katika uchaguzi mkuu ujao atakapowania kiti cha urais pale aliitaka jamii ya Wakamba kuiga mfano wake na pia kujitenga na viongozi ambao hawana malengo ya kuwatumikia.
"Kwa hali na mali, kiangazi au Masika nitasimama na Kalonzo Musyoka hadi mwisho hata nipo tayari kupoteza chochote nkiwa naye," alikiri Muthama.
Naye Kamishna wa bondi ya uchaguzi ya chama cha Cord kutoka Ukambani Peter Mutulu akizungumzia katika hafla tofauti eneo la Mwala alielezea kushangazwa kwake baada ya tume ya IEBC kudai kuwa kati ya sahihi millioni moja nukta sita zilizowasilishwa na chama cha Cord ni sahihi elfu mia name na tisini na moja nukta sita tu zilizo halali.