Share news tips with us here at Hivisasa

Huku tarehe ya uchaguzi mdogo wa Malindi ikikaribia, joto la kampeni linazidi kupanda eneo hilo huku kila upande ukionyesha ubabe wake.

Licha ya kwamba kuna wagombea kadhaa wanaowania kiti hicho cha ubunge kupitia vyama mbalimbali, mirengo wa Cord na Jubilee inaonekana kuwa na ushawishi mkubwa zaidi.

Mapema siku ya Ijumaa mfuasi wa Cord ambaye pia ni mwakilishi wa Wadi ya Mwareni Kassim Mwapojo alikamatwa na polisi na kuzuiliwa kwa saa kadhaa kabla kuachilia baada ya wanachama wa Cord kuingilia kati.

Mwapojo alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Malindi ambapo wanachama wa ODM baadae walikita kambi katika kituo hicho na kushinikiza kuachiliwa kwake.

Kinara wa Cord Raila Odinga anayeongoza ODM katika kampeni hizo alilaani kitendo hicho huku akinyosha kidole cha lawama kwa Jubilee kwa kudai kuwa walihusika katika jambo hilo.

Kiongozi wa chama cha Wiper ambaye pia ni mmoja wa vinara wa Cord Kalonzo Musyoka pia alikerwa na hatua hiyo.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho naye alitaja kitendo cha kukamatwa kwa Mwapojo kama mbinu ya Jubilee ya kuzima ODM dhidi ya kushinda uchaguzi huo baada ya kugundua kwamba watashindwa.

Kupitia kwa mitandao yake ya kijamii, Joho alisema kuwa polisi hawakuwa na sababu yoyote ya kumkamata na hiyo inaonyesha wazi kwamba ilikuwa ni njama tu.

“Baada ya kuhisi kwamba tutawashinda, sasa Jubilee wameanza mbinu ya kuwakamata wafuasi wakuu wa chama chetu bila hata kutoa sababu za kueleweka,” alisema Joho.

Joho aidha alisema kuwa wanalaani kitendo hicho na kuongeza kuwa hizo ni mbinu za zamani zilizopitwa na wakati hapa nchini.

Uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi unatarajiwa kufanyika tarehe 7 mwezi huu wa Machi sawa na na ule wa Kaunti ya Kericho ambapo pia watakuwa wakimchagua seneta mpya.

Kiti cha ubunge cha Malindi kiliachwa wazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Dan Kazungu kama waziri wa madini.