Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia visa vya watu kujiua kuendelea kuripotiwa katika Kaunti ya Nyamira, OCPD wa Nyamira Rico Ngare, amejitokeza kuhimiza viongozi wa makanisa kuwashauri vijana dhidi yakustahimili wanapozongwa na mawazo.

Kwenye mahojiano na wanahabari ofisini mwake siku ya Jumanne, Ngare alisema ni jambo la kushangaza idadi kubwa ya vijana wanapoendelea kujitoa uhai wakiwa na umri mdogo ikizingatiwa wao ndio viongozi wa siku za usoni

"Hatutaki kusikia ripoti za watu kujitoa uhai na ni himizo langu kwa viongozi wa makanisa kuweka mikakati ya kuwa na vitengo maalum kanisani, ili kuwapa ushauri waumini wao dhidi ya kujinasua kutoka kwa matatizo yanayoweza kuwasababisha kujiua," alisema Ngare.

Aliongeza, " Ni jambo la kushangaza kubaini kuwa idadi kubwa ya vijana wanaendelea kujitoa uhai kwasababu ya shida zao za kibinafsi. Hali hiyo inalinyanganya taifa hili viongozi wa kesho."

Kisa cha hivi maajuzi kiliripotiwa katika eneo la Marindi, wilayani Nyamira Kusini, pale ambapo mwanamume wa umri wa makamo alipatikana akininginia mtini siku ya Jumatatu.

Afisa huyo aidha alisema mwili wa mwendazake unaendelea kuhifadhiwa kwenye Hospitali Kuu ya Nyamira, huku maafisa wa polisi wakianzisha uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.