Katibu muandalizi wa Baraza la Maimamu nchini (CIPK) Sheikh Mohammed Khalifa amekashifu kitendo cha wapenzi wa jinsia moja kuandamana jijini Mombasa hivi maajuzi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Sheikh Khalifa ameonesha kugadhabishwa na tukio hilo ambapo wapenzi wa jinsia moja waliandama kupinga kubaguliwa katika vituo vya afya.

"Ni jambo la kusikitisha kuwaona wapenzi wa jinsia moja wakiingia jijini wakitangaza vitendo vyao ambavyo ni kinyume cha maadili. Sisi kama viongozi wa dini tunaomba vyombo vya habari viwapuuzilie mbali na kutopea maslahi yao kipao mbele," alisema Khalifa.

Akiongea katika ukumbi wa shule ya Kenya School of Government siku ya Jumatano, Sheikh Khalifa alitoa tahadhari kuwa endapo jamii itakubali mapenzi ya jinsia moja, nchi itaangamia.

"Hakuna haki ya binadamu kinyume na maamrisho ya mungu. Ni mzazi gani duniani anapenda mtoto afanye ushoga? Ikiwa mapenzi ya jinsia moja ni haki ya binadamu, basi pia wahuni watakuwa na haki ya kuiba na kuharibu mali ya watu. Hiyo ni kinyume cha maadili na dini," alisema Khalifa.

Wakati huo huo, Sheikh Khalifa alitoa changamato kwa kina mama na wasichana wanaojihusisha na biashara ya ukahaba.

"Ikiwa mama anafanya ukahaba kwa madai ya kupata karo za masomo ya mtoto wake, je yule mtoto atakapo fanya ile biashara atakuwa amekosea ilhali tayari anafahamu mamake anajihusisha na biashara hio?” aliuliza Khalifa.

Kwa upande wake, Askofu Jacob Kosgey aliyakosoa mashirka ya kigeni yanayopigania haki za wapenzi wa jinsia moja.

"Tunajua kuna mashirika yatatia nguvu kurekebishwa kwa katiba ili kuruhusu ndoa ya jinsia moja. Hatutaruhusu hilo kwani ndoa ni kati ya jinsia mbili tofauti,” alisema Kosgey.