Muungano wa makanisa nchini umepongeza hatua iliyochukuliwa na viongozi wa mrengo wa Cord kusitisha maandamano ya kila Jumatatu dhidi ya Tume ya IEBC kwa muda ili kutoa nafasi kwa majadiliano na serikali.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa muungano huo eneo la Pwani Askofu Joseph Maisha, alisema tangu Cord ianzishe maandamano ya kushinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kumeshuhudiwa visa vya maafa na makabiliano yanayotishia kuleta mgawanyiko nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Askofu Maisha aliwahimiza viongozi wa kisiasa humu nchini kuiheshimu katiba na kujishugulisha zaidi na masuala ya maendeleo.

“Tunaunga mkono hatua ya Cord kusitisha maandamano na tunawaomba kuheshimu katiba ya nchini na kufanya mambo yao ya kisiasa kwa misingi ya kujali maisha ya Wakenya wanyonge,” alisema Askofu Maisha.

Mrengo wa Cord ulisema kuwa utasitisha maandamano yake ya kila Jumatatu kwa muda hadi tarehe Juni 6, ili kutoa nafasi kwa mazungumzo na serikali.