Baada ya athari za mafuriko kushuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya eneo la Pwani kufuatia mvua kubwa iliyonyesha, sasa viongozi wa dini wanatoa shinikizo kwa Serikali za kaunti za Pwani itafute suluhisho la kudumu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini Kaunti ya Kwale, Faraj Abubakar Omar, alisema kuwa japo wakazi wamekuwa wakitoa lalama zao kwa viongozi wao, hakuna juhudi zinazoendelezwa kuidhibiti hali hiyo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa baada ya mkutano wa kidini na viongozi wa baraza hilo, Ustadh Omar, alisema kuwa sio vyema kwa serikali za kaunti za Pwani kulifumbia jicho tatizo hilo linalochangia hasara za mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua.

Ustadh Omar alisisitiza kuwa wao kama viongozi wa dini hawatalinyamazia suala hilo hadi pale serikali kuu na zile za kaunti za Pwani zitakapo liwajibikia tatizo hilo.

“Tunashindwa kuelewa hawa viongozi wetu hapa Pwani, yaani imeonekana kulisahau kabisa tatizo linalowapitia wakaazi waliwachagua na kuwaacha wakaazi wakipitia harasa kubwa kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua, lazima swala hilo kutatuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema Ustadh Omar.

Mafuriko hayo ya wiki jana yalikumba maeneo kadha katika ukanda wa Pwani ikiwemo Wadi ya Vanga, Tana River, Mombasa na maeneo mengine ya Pwani.