Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Garissa wametoa hisia tofauti baada ya serikali kutangaza kuwa kambi ya wakimbizi ya Daadab itafungwa miezi michache ijayo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Hatua hii iliafikiwa na serikali baada ya kambi hiyo kudaiwa kuwa uwanja wa mazoezi ya wana mgambo wa Alshabaab, ambao wanatishia usalama wa Wakenya.

Wakizungumza huko Garissa, viongozi hao walitoa hisia zao, huku wengine wakiunga serikali mkono na wengine kuonekana kupinga hatua hiyo. 

Seneta wa Garissa Yussuf Haji alisema kuwa iwapo hatua hiyo itatekelezwa, wakimbizi hao watashinikizwa kujiunga na kundi la Alshabaab.

“Wakimbizi wamekuwa hapa kwa zaidi ya miaka 30, wanaelewa kiswahili na lugha zingine. Wanajua kila sehemu ya Kenya,” alisema, akiongezea kuwa kuwatimua kwa nguvu itawaweka katika hatari ya kujiunga na ISIS na Alshabaab.

Seneta Haji alisema kuwa wengi wa wakimbizi hao wamepata vitambulisho ya Kenya na iwapo watatimuliwa kwa nguvu, watahatarisha usalama wa Wakenya kwa kiasi kikubwa.

Mwakilishi bunge wa Ijara Ahmed Ibrahim kwa upande wake aliunga hatua ya serikali huku akisema kuwa ni heri warudishwe Somalia kwa sababu ya usalama.

Mbunge wa Daadab Mohamed Dahiye alisema kuwa ni ishara ya kukosa utu iwapo serikali itawafurusha wakimbizi hao, na kusisitiza kuwa hatua hiyo haifai na ya kuwa haitawezekana kuwafurusha zaidi ya watu elfu mia tatu kwa miezi sita.

Dahiye alisema kuwa kuna maelfu ya Wakenya ambao majina yao yamenaswa na UNHCR kama wakimbizi, licha ya kuwa wao si wakimbizi na wanafaa kupewa stakabadhi za kuwatambua kama Wakenya.