Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar pamoja na viongozi wengine wa Jubilee kutoka ukanda wa Pwani wakiwahutubia wanahabari. [Picha/ the-star.co.ke]
Viongozi wa chama cha Jubilee wamepinga mpango wa viongozi wa NASA wa kutaka eneo la Pwani kujitenga kutoka Kenya.Kwenye kikao na wanahabari wakiongozwa na Waziri wa Utalii Najib Balala, viongozi hao walisema kuwa eneo la Pwani litasalia kuwa Kenya.Balala amesisitiza kuwa hawatakubali harakati zozote za kujitenga kwa Pwani.“Hatutakubali kamwe Pwani kujitenga kwa sababu eneo hili bado ni Kenya na litasalia kuwa Kenya,” alisema Balala.Balala amemtaja Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kama wenye malengo ya kutaka kujitajirisha kibinafsi na sio kuwatumikia wananchi.“Joho na Kingi hawana malengo ya maendeleo bali wanataka kujinufaisha kibinafsi bila kujali walalahoi,” alisema Balala.Balala vile vile amewataka magavana hao wawili kuweka wazi jinsi walivyotumia zaidi ya shilingi bilioni 100 walizopokea kutoka kwa serikali kuu.Kwa upande wake, Gavana wa Kwale Salim Mvurya alisema kuwa vitisho hivyo vya kujitenga kwa Pwani vimeanza kuzua hofu miongoni mwa wakaazi.“Wakaazi wengi wameingiwa na hofu tayari kuhusu madai yaliyotolewa na viongozi hao wawili. Wizi wa mashamba umeanza kufichuka,” alisema Mvurya.Mvurya amewataka Joho na Kingi kuonyesha wapwani yale waliyowafanyia wananchi wao kabla ya kuanza harakati ya kujitenga.“Acheni porojo zisizokuwa na maana. Wekeni wazi miradi muliyofanyia wananchi wenu kwa muda ambao mumekuwa madarakani,” alisema Mvurya.Naye aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar amesema katiba hairuhusu Pwani kujitenga na kuitaja hatua hiyo kama njama ya kuhujumu katiba.Aidha, alidai kuwa hatua hiyo ya viongozi wa NASA ni njama ya kuzua fujo na kutatiza amani eneo la Pwani.“Hawa jamaa wanapanga kuzua fujo na kutatiza amani inayoshuhudiwa eneo nzima la Pwani. Hawana mwelekeo wowote wa maana,” alisema Omar.