Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kanisa nchini wamepinga hatua ya Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kupiga marufuku hafla ya maombi shuleni wakati wa masomo ya muhula watatu kama njia mojawapo ya kuzuia wizi wa mtihani.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, Naibu Askofu wa kanisa la Katoliki dayosisi ya Mombasa, Wilybard Lagho, alieleza kushangazwa na marufuko hayo huku akimtaka waziri kutoa ushahidi unaohusisha maombi na wizi wa mtihani.

“Ni vyema waziri athibitishe kwa ushahidi kuwa kiongozi wa kanisa fulani alihusika na wizi wa mtihani wakati wa maombi. Ikiwa kunayo, basi shule hiyo ipigwe marufuku lakini sio kuadhibu shule zote,” alisema Lagho.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa kidini alisema kuwa kama kanisa wanaunga mkono juhudi za Matiang'i kuziba mianya yote inayotumika kueneza wizi wa mtihani nchini.

“Tunamuunga mkono waziri katika harakati na juhudi zake kuvikabili visa vya wizi wa mtihani. Ni jambo ambalo lazima likomeshwe lakini kwa njia inayokubalika,” aliongeza Lagho.

Mapema wiki iliyopita, Waziri wa Elimu Fred Matiang’i alipiga marufuku hafla za maombi pamoja na ziara za wazazi shuleni wakati wa masomo ya muhula wa tatu kama njia mojawapo inayolenga kupunguza wizi wa mtihani miongoni mwa watahiniwa.