Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa baraza la dini mbali mbali Pwani wameahidi kushirikiana na wakuu wa usalama katika Kaunti ya Mombasa kuvikabili visa vya utovu wa usalama katika eneo hilo.

Wakiongozwa na mchungaji Stephen Anyenda siku ya Jumanne, viongozi hao walikubali kushirikiana na idara ya usalama pamoja na viongozi wa kisiasa ili kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakumba eneo la Pwani.

“Kama wahubiri na waumini, tuko tayari kufanya kazi na walinda usalama ili kuhakikisha kuwa eneo la Pwani liko salama kwa wananchi wote. Naamini tukishirikiana tutaweza kuyapa suluhu matatizo yanayowakumba wakaazi,” alisema Anyenda.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki aliwahimiza viongozi hao wa kidini kuisaidia idara ya usalama kutokomeza imani potovu inayochangia vijana kujiunga na makundi haramu na kisha kuhatarisha usalama mjini humo.

“Nanyi kama viongozi wa kanisa nawasihi mtusaidie kulikabili suala hili la itikadi kali miongoni mwa waumini, ili tuweze kumaliza mambo haya ya vijana kujihusisha na makundi haramu,” alisema Achoki.

Aidha, Achoki alisema kuwa visa vya utovu wa usalama ambavyo vilikithiri katika maeneo mbalimbali mjini Mombasa mapema mwaka huu hasa Likoni na Kisauni kwa sasa vimepungua kutokana na usalama ulioimarishwa na maafisa wa polisi.