Muungano wa makanisa ya kiivangelisti nchini umehimiza amani na utulivu wakati uchaguzi mkuu ujao ukikaribia.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwahutubia wanahabari mjini Nakuru Jumanne baada ya kukamilika kongamanao la siku mbili lilowaleta pamoja maaskofu wa muungano, Askofu Mark Kariuki alisema kuwa kuna umuhimu wa viongozi wa kidini na wale wa kisiasa kuwaunganisha wananchi ili kurejesha amani na utulivu.

"Sisi letu tu ni kuwarai viongozi wa kisiasa kukoma kuliyumbisha taifa hili na semi zao na badala yake washirikiane katika kunena usemi wa amani na maridhiano,"alisema askofu Kariuki.

Wakati huo huo alitoa wito kwa tume ya uwiano na maridhiano -NCIC- kuhakikisha kwamba inawachukulia hatua kali wale wote wanaoeneza semi za chuki.

Kwa mujibu wake, ni semi kama hizo ambazo zinaweza kuyumbisha taifa na kusababisha machafuko kama yale yaliyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

"Ni jambo la kusikitisha kwa viongozi wa kisiasa kuendelea kutoa matamshi ya kuliyumbisha taifa hili na ndiposa tunatoa wito kwa taasisi husika kuhakikisha kwamba zinatekeleza wajibu wao katika kuwaadhibu wale ambao wanaeneza chuki na uhasama.

Matamshi haya yalijiri wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu swala la tume huru ya uchaguzi na mipaka humu nchini IEBC.