Viongozi wa kidini mjini Mombasa sasa wanataka maafisa wa polisi kusitisha disko za usiku mjini humo, kwa madai kuwa kesha hizo ndizo huchangia vijana kujihusisha na maovu ikiwemo anasa, uhalifu na utumizi wa mihadarati.
Wakizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, walisema kuwa vijana wengi mjini Mombasa hutumia fursa hiyo kufanya visa vya kihalifu na kuchangia hofu ya ukosefu wa usalama miongoni mwa jamii.
Sheikh Khalifa alipendekeza kusitishwa kwa disko za usiku sambamba na vijana kuonywa dhidi ya kuhudhuria mikahawa mjini humo.
Alisema kuwa iwapo vijana watapatikana katika hafla hizo, basi hatua za kisheria zichukuliwe mara moja dhidi yao ili mji wa Mombasa uwavutie wageni wengi.
"Tungependa kuwaambia maafisa wa polisi kuchukua hatua za haraka na kusitisha disko za usiku katika mji wa Mombasa ili kuzuia vijana wadogo kujitosa katika maswala ya kihalifu na mihadarati. Bila ya kufanya hivyo, basi ukosefu wa usalama utakithiri,” alisema Sheikh Khalifa.