Huku Waislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid-ul-adha, viongozi wa dini ya Kiislamu wamelaani vikali shambulizi la kigaidi katika Kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa.
Kadhi mkuu nchini Sheikh Ahmed Muhdhar, amesema kuwa tukio la siku ya Jumapili mjini Mombasa ni la kigaidi na lazima likomeshwe, kwani ni aibu mno kwa dini ya Kiislam kwa mwanamke kujiunga na ugaidi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Sheikh Muhdhar alisema kuwa visa kama hivyo havitovumiliwa na Wakenya, kwani ni hatari zaidi kwa usalama wa nchi.
Kiongozi huyo wa dini ameitaka idara ya usalama kuweka mikakati mwafaka ili kukabiliana na magaidi.
"Tunalaani kitendo cha ugaidi cha siku ya Jumapili na tunaihimiza serikali kuweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na magaidi,” alisema Muhdhar.
Wakati huo huo, amewataka Wakenya kudumisha amani na kushirikiana na maafisa wa polisi katika kuthibiti usalama, kwa kuripoti visa vya kihalifu ili wahalifu na magaidi wakabiliwe kisheria.