Baraza la Maimam na Wahubiri nchini CIPK, limesema litashirikiana na idara ya usalama katika vita dhidi ya itikadi kali na makundi ya uhalifu mjini humo.
Baraza hilo limesema kuwa litajitokeza na kutoa mafunzo kwa vijana wa eneo hilo kwa kuwa hao ndio walio kwenye tishio la kujiunga na makundi hayo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohamed Khalifa, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona watoto wanajiunga na uhalifu na kukiuka maadili.
“Inasikitisha kuwaona watoto wadogo wakijihusisha na ujambazi na kubeba mapanga na visu wakipiga watu badala ya kwenda shuleni au katika madrassa,” alisema Sheikh Khalifa.
Kiongozi huyo alisema tatizo hilo limeathiri zaidi Kaunti ya Mombasa ikilinganishwa na maeneo mengine ya ukanda wa Pwani.
Sheikh Khalifa aidha alisema kuwa dini ya Kiislamu hairuhusu ugaidi wala misimamo mikali na kushangazwa na jinsi vijana wengi wamekuwa wakipotoshwa.
“Katika kaunti yetu kuna watu walioathirika na fikra za kigaidi na hiyo ni misimamo isiyokubaliana na misingi ya Kiislamu kabisa,” alisema Khalifa.
Kauli ya Sheikh Khalifa imeonekana kuleta matumaini makubwa katika vita dhidi ya uhalifu baada ya eneo hilo kutajwa kukumbwa na changamoto kubwa.
Serikali imekuwa ikishinikiza viongozi wa kidini kujitokeza na kusaidia katika vita dhidi ya ugaidi kwani viongozi hao wameonekana kuwa na ushawishi mkubwa na juhudi zao huenda zikasaidia kukomesha janga hilo.