Wito umetolewa kwa viongozi wa kisiasa katika Kaunti ya Kisumu kusitisha migogoro kati ya viongozi wa serikali ya kaunti hiyo na bunge la Kaunti ya Kisumu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa vuguvugu la wenyeji wa jiji la Kisumu, (Kisumu City Residence Voice), Audi Ogada, amesema wengi wa viongozi wa Kaunti ya Kisumu wameishia kupotelea katika malumbano ya kila mara badala ya kuzingatia na kushugulikia maswala muhimu yatakayowasaidia wenyeji waliowachagua ili kuwawakilisha.

Ogada ameshikilia kuwa wakaazi wa Kaunti ya Kisumu wamechoshwa na vita baina ya viongozi hao, hasaa ikizingatiwa kuwa mivutano kati yao imekuwa ikijirudia kila mara bila utatuzi mwafaka kuafikiwa.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa wametoa makaata ya siku mbili kwa viongozi hao kutafuta mbinu za kutatua tofauti zao hasaa kuhusiana na swala la kusimamishwa kazi kwa meneja wa jiji la Kisumu Dorice Ombara, ambaye tayari amepewa majukumu mengine katika idara tofauti, la sivyo wajiuzulu kutoka nyadhifa zao.

Ogada alisema kuwa wakaazi wa Kisumu hawataruhusu misuko suko ya viongozi wao inayoendelea kwa sasa kurudisha nyuma hatua na juhudi za maendeleo.

“Mvutano uliopo kati ya serikali ya Kaunti ya Kisumu na meneja wa jiji la Kisumu unalenga kutatiza utoaji wa huduma kwa wakaazi, kwahivyo ipo haja kwa swala hili kutatuliwa kwa haraka. Baada ya siku mbili itabidi wakazi tushiriki maandamano na kutumia mbinu zingine za kisheria kuwasilisha lalama zetu,” alisema Ogada.