Mwenyekiti wa chama cha maktaba nchini Samuel Nyangeso amewaomba viongonzi wote wa eneo la Kisii walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika mashirika mbalimbali ya serikali hivi maajuzi kuungana pamoja na kutafuta njia ya kuinua jamii ya wakisii.
Alikuwa akiyaongea haya mnamo siku ya Ijumaa kwenye hafla ya kufadhili shule ya upili ya Nyamoya iliyoko eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii vitabu.
“Nawaomba wale walioteuliwa na rais katika mashirika ya serikali, ingawa mliteuliwa kuwatumikia wakenya wote, ni heri mkumbuke mlikotoka kwa jamii ya Wakisii, ili jami yetu iinuke kimaendeleo, kielimu na mambo mengine, nawaomba tuungane pamoja tuinue jamii yetu,” alitaja Nyangeso.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo aliwaomba viongonzi wote waliochaguliwa na wananchi kuweka siasa kando na kuwatumikia wananchi na kufanya maendeleo katika sehemu zao.
“Wale mliochaguliwa jaribu muwezalo kufanya maendeleo na kutimiza yale mliowahidi wananchi wakati wa kampeni ,” aliongezea Nyangeso.
Aidha, mwenyekiti huyo alisema hakuna haja ya kuwarejesha uongozini wale hawatimizi ahadi walizohaidi.
“Awe gavana, awe mbunge na hata mwakilishi wa wadi, kama hatimizi na kufanya maendeleo hatarejeshwa mamlakani kamwe, viongonzi hao walichaguliwa kufanya maendeleo kwa wananchi,” alisema Nyangeso.