Mbunge wa Homabay Town amewataka viongozi wote kutoka eneo pana la Nyanza Kusini ikiwemo Kisii kuunga mkono pesa za maendeleo ya maeneo bunge CDF, ili zibaki katika mikono ya wabunge.
Akiongea hii leo kwenye hafla ya kukusanya maoni kutoka kwa wakaazi wa kaunti za Kisii, Migori na Nyamira ambayo ilifanyiwa kwenye ukumbi wa umma wa Cultural Centre, Kaluma alisisitiza umuhimu wa pesa hizo ambazo alisema kuwa zimesaidia pakubwa kwa kuinua maendeleo ya maeneo ya mashinani.
“Pesa hizo sharti zibaki na kujumuishwa katika katiba mpya, zikiwekwa katika mikono ya mawaziri sitakuwa na mda wa kuenda kwa Prof Kaimenyi kumuomba pesa eti choo cha shule flani kimeporomoka na kinahitaji kujengwa,” alihoji Kaluma.
Aliahidi kupigana hadi mwisho kuhakikisha pesa hizo zinabaki chini ya mamlaka ya wabunge, na kuona kuwa zinasimamiwa vizuri na pia kudokeza kuwa atasimamia mswada ambao utahakikisha kuwa matapeli ambao wamekuwa wakiwekwa na viongozi flani kusimamia pesa hizo wanaondolewa ili kulisafisha jina la usimamizi wa pesa hizo.
Pesa za maendeleo ya maeneo bunge zimekuwa na mzozo kati ya maseneta na magavana, huku wengi wa wananchi na viongozi wakitaka sheria maalumu kuwekwa ili kutoa uangalizi na usimamizi ulio wazi wa fedha hizo ambazo licha ya kufanya maendeleo katika mashinani, zimelaumiwa kwa kutoa mwanya kwa wabunge wengi kuwa wafisadi na kuwaajiri jamaa zao kusimamia miradi inayofadhiliwa na hela hizo.