Kamishna wa kaunti ya Nyamira Bi Josphine Onunga amewaomba viongozi wa makanisa kwenye Kaunti ya Nyamira kuwa kwenye mstari wa mbele kueneza ujumbe wa amani na utangamano.
Kamishna Onunga alisema kuwa wakati mwingi viongozi wa makanisa huwa na ushirikiano wa karibu na wakristu wa madhehebu yao akiongeza kusema kuwa viongozi hao wana wakati mzuri wakueneza ujumbe wa amani miongoni mwa wakristu hao.
"Viongozi wa makanisa huwa na wakati mwingi pamoja na washirika wao na yafaa wawe kwenye mstari wa mbele kuhakikisha kuwa ujumbe wa amani umeenezwa miongoni mwa washirika hao,” alisema Onunga.
Akihutubu kwenye kikao cha ufunguzi wa mkutano wa siku nne kuhusu uhamasisho baina ya viongozi wa makanisa kule Nyamira siku ya Jumatatu, Onunga alisema kuwa utangamano na amani ni vigezo muhimu katika uimarishaji wa uchumi nchini na kwahivyo yafaa kuzingatiwa.
"Utangamano na amani ni vigezo muhimu sana katika uimarishaji wa uchumi hasa kwa mataifa yanayostawi na kwa hivyo lazima yazingatiwe," alisema Onunga.
Naibu mkurugenzi wa tume ya utangamano nchini Edward Nyongeza alisema kuwa tume hiyo imekita kambi kwenye kaunti ya Nyamira kwa siku nne zijazo ili kuhamasisha viongozi wa makanisa kuhusiana na umuhimu wa amani.
Alisema kuwa mikutano sawia na hiyo imefanywa kwenye kaunti ya Kisii, Migori na Homa-bay.
"Tume ya utangamano imekita kambi humu Nyamira kwa siku nne ili kuwahamasisha viongozi wa makanisa kuhusiana na umuhimu wa amani na utangamano,” alisema Nyongeza.