Mkurugenzi wa shirika moja la kidini nchini linalohamazisha wananchi kuhusu haki na amani la Ecumenical Centre for Peace and Justice (ECJP) tawi la Kisumu Elias Komenya amehimiza wananchi kusameheana na kutangamana ili kuleta maendeleo nchini.
Akihutubu katika Wadi ya Manyata mjini Kisumu kwenye kongamano la Ward Peace Forum na viongozi wa kidini mnamo siku ya Alhamisi, Komenya aliwataka viongozi wote wa kidini kuhubiri amani na utangamano makanisani ili kumaliza nyongo na uhasama miongoni mwa wananchi.
Kiongozi huyo wa kidini aliwataka wananchi kujifunza kusameheana na kusahau yaliyopita, akisema kuwa maendelo ya kila mmoja yanategemea amani na umoja.
Alisema kuwa taifa la Kenya lina kabila nyingi na kila mmoja anapaswa kujifunza kuishi kwa njia ya amani na upendo huku akitaka kila mmoja kutenda haki.
Komenya alihoji kuwa wananchi wengi nchini wangali na nyongo mioyoni mwao tangu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 ambapo ghasia zilishuhudiwa baada ya uchaguzi.
Alisema kuwa hali kama hiyo haitakikani tena kutokea licha ya kuwepo kwa makanisa na wahubiri wengi nchini ambao wamebeba majukumu ya kuhubiri matendo mema miongoni mwa jamii.
“Hatupaswi kulaumiwa kama kanisa kwa kuzembea kazini mwetu ilhali tumepewa nafasi na uhuru wa kuhubiri na kuabudu. Tuitumie nafasi hiyo vyema ili kuwepo haki na amani miongoni mwa wakenya,” alisema Komenya.
Aidha Mkurugenzi Komenya pia alitaka Serikali ya Kaunti ya Kisumu kuwatendea wenyeji wa eneo hilo haki wakati wanapotafuta haki kwenye maswala ya kisheria, akisema kuwa kukosa kuwatendea wananchi haki kwenye maswala hayo pia huongeza uhasama miongoni mwao.