Viongozi wa makanisa wametaka mgogoro kuhusu Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC kusuluhishwa kwa njia ya amani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza siku ya Jumanne, baada ya mkutano na viongozi wa muungano wa Cord katika afisi ya Raila Odinga mjini Nairobi, viongozi hao wa kidini waliutaka muungano huo kusitisha maandamano yao ya kila wiki.

Hata hivyo, vinara wa Cord walikataa wito huo na kusema kuwa maandamano hayo yataendelea mpaka pale tume hiyo itakapoondoka mamlakani.

"Lengo letu ni kupata suluhu la amani na tumekuja hapa kujadili njia mwafaka ya kusuluhisha mgogoro huu ili keupukana na fujo. Tunapaswa kujifunza kutoka kwa makosa yetu ya hapo awali ili tusiyarudie,” alisema Askofu Cornelius Korir.

Korir alisema kuwa ipo haja ya kuwahusisha wadau tofauti ili kuhakikisha kuwa mgogoro huo wa IEBC unatatuliwa kwa njia ya amani.

Viongozi hao wa kanisa wanatarajiwa kukutana na makamishna wa Tume ya IEBC pamoja na viongozi wa serikali siku ya Jumatano.