Baadhi ya viongozi wa vijana kutoka kaunti ya Nyamira wamejitokeza kushtumu hatua ya viongozi wa kaunti ya Nyamira kutohudhuria kongamano la kibiashara liloandaliwa katika kaunti ya Kisii.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Nyambega Gisesa, vijana hao walishtumu vikali hatua ya viongozi wakuu wa kaunti kutohudhuria kongamano hilo, huku wakitaja hatua hiyo kama ya aibu kubwa.

“Ni jambo la aibu kuwa viongozi wetu walikosa kuhudhuria kongamano la kibiashara kule Kisii ilhali tunataka kujiendelesha kama kaunti kwa misingi ya kunawiri kwetu kiuchumi na hata pia kisiasa, na tunahitaji viongozi wanaoshirikiana wengine ili kujistawisha,” alisema Gisesa.

Nyambega aidha aliwataka viongozi wa serikali ya kaunti ya Nyamira kuchukua hatua za kutembelea kaunti ya Kisii ili kusoma mengi kuhusiana na kongamano hilo, hali itakayowaruhusu viongozi hao kuandaa kongamano la kibiashara sawia na hilo.

“Nawashauri viongozi wa kaunti hii kuchukua hatua ya kutembelea kaunti ya Kisii ili kupata maarifa kuhusiana na kongamano la kibishara kwa kuwa tutahitaji kuona kaunti hii ikiiga mfano wa kaunti ya Kisii kwa maana tunataka kustawi,” aliongezea Gisesa.